“Yeye Ambaye ni Bwana wenu, Mwenye-Rehema Zote, huthamini moyoni Mwake shauku ya kuona mbari nzima ya binadamu kama roho moja na mwili mmoja.”— Bahá'u'lláh

Katika maelfu kwa maelfu ya maeneo kote ulimwenguni, mafundisho ya Imani ya Kibahá’í yanawavutia watu binafsi na jumuiya wanapojitahidi kuboresha maisha yao wenyewe na kuchangia kwenye uendelezaji wa ustaarabu. Itikadi za Kibahá’í hushughulikia mada muhimu sana kama vile umoja wa Mungu na dini, umoja wa binadamu na uhuru kutokana na chuki au mapenzi yasiyo na sababu, asili bora ya mwanadamu, ufunuo uendeleao wa ukweli wa kidini, ukuzaji wa sifa za kiroho, muungano wa ibada na huduma, usawa wa kimsingi wa jinsi, upatano kati ya dini na sayansi, umuhimu mkuu wa haki katika jitihada zote za kibinadamu, umuhimu wa elimu, na mienendo ya uhusiano ambao utawaunganisha pamoja watu binafsi, jumuiya, na asasi, kadri jamii ya binadamu isongavyo mbele kuelekea ukomavu wake wa pamoja.

Eneo hili la tovuti linalenga kupanga uteuzi wa itikadi muhimu za Kibahá’í katika maeneo kadhaa ya maudhui— Maisha ya Roho; Mungu na Muumbo Wake; Uhusiano Muhimu sana; na Amani ya Ulimwengu. Aidha, sehemu yenye kichwa cha habari Bahá’u’lláh na Ahadi Yake hutoa muhtasari wa vyanzo vya Imani ya Kibahá’í, ikijumuisha maelezo mafupi ya Maisha ya Báb, Bahá’u’lláh, ‘Abdu’l-Bahá, and Shoghi Effendi. Pia inatambulisha Nyumba ya Haki ya Ulimwengu, asasi iliyoamriwa na Bahá’u’lláh ambapo leo jumuiya nzima ya Wabahá’í hugeukia kwa ajili ya mwongozo kwenye kuweka katika vitendo mafundisho ya Kibahá’í.

Ili kupata utambuzi kamili wa itikadi za Kibahá’í huenda utataka kutembelea Maktaba ya Kibahá’í ya Marejeo ambako unaweza kusoma Maandiko ya Báb, Bahá’u’lláh, na ‘Abdu’l-Bahá pamoja na juzuu zilizoandikwa na Shoghi Effendi na teuzi la matamko na mawasiliano ya Nyumba ya Haki ya Ulimwengu.

Enyi watoto wa watu! Kusudi la kimsingi linalohuisha Imani ya Mungu na Dini Yake ni kuhifadhi manufaa na kukuza umoja wa jamii ya binadamu, na kuendeleza moyo wa upendo na undugu miongoni mwa watu….Chochote kiinuliwacho juu ya msingi huu, mabadiliko na nasibu za ulimwengu haziwezi kamwe kudhuru nguvu yake, wala mzunguko wa karne zisizohesabika kudhoofisha muundo wake.

— Bahá'u'lláh