“Kikombe cha ujuzi kinafurika; wamebarikiwa wale wanaoshiriki mafunda! Chemchemi ya uzima inabubujika nje; wamebarikiwa wale wanaokunywa!”— ‘Abdu’l‑Bahá

Tangu mwanzo wa Imani ya Kibahá’í Karne ya Kumi na Tisa, idadi inayoongezeka ya watu wamepata ndani ya mafundisho ya Bahá’u’lláh maono ya kuvutia sana ya ulimwengu ulio bora zaidi. Wengi wamechota umaizi kutoka mafundisho haya—kwa mfano, juu ya umoja wa binadamu, juu ya usawa wa wanawake na wanaume, juu ya uondoaji hisia za chuki au mapenzi ya bila sababu, juu ya upatano wa sayansi na dini—na wamejaribu kutumia kanuni za Kibahá’í katika maisha yao na kazi. Wengine wameenda mbali zaidi na wameamua kujiunga na jumuiya ya Kibahá’í na kushiriki katika jitihada zake kuchangia moja kwa moja kwenye utimizwaji wa maono ya kustaajabisha ya Bahá’u’lláh juu ya ukomavu wa jamii ya binadamu.

Wabahá’í wanatoka matabaka yote ya jamii. Vijana na wazee, wanaume na wanawake kadhalika, wanaishi sambamba na wengine katika kila nchi na wanatokea katika kila taifa. Wote wana lengo moja la kuhudumia jamii ya binadamu na kuboresha maisha yao ya ndani kufuatana na mafundisho ya Bahá’u’lláh. Jumuiya ambayo wanatokea ni moja ya kujifunza na kutenda, huru kutoka hisia yoyote ya kiburi au madai ya kuwa na uelewa wa pekee wa ukweli. Ni jumuiya inayojitahidi kukuza matumaini ya wakati ujao wa binadamu, kuendeleza jitihada zenye madhumuni, na kusherehekea juhudi za wale wote ulimwenguni wanaofanya kazi kujenga umoja na kuondoa mateso ya wanadamu.

Bahá’u’lláh amechora duara ya umoja, Ameunda mpango kwa muungano wa watu wote, na kwa ukusanyikaji wao chini ya kimbilio la hema la umoja wa kiulimwengu. Hii ni kazi ya Maajaliwa Matakatifu, na inatubidi sisi sote kujitahidi kwa moyo na roho mpaka tuwe na uhalisi wa umoja miongoni mwetu, na jinsi tunavyofanya kazi, ndivyo tutapewa nguvu.

— ‘Abdu’l‑Bahá