Kile Wabahá’í wanachofanya
Vijana
Nyenzo kutoka kwenye makongamano ya vijana
Uchangiaji kwenye Uendelezaji wa Ustaarabu
Miongoni mwa mada zilizochunguzwa wakati wa mfululizo wa makongamano ya vijana duniani kote mwaka 2013 na mawimbi ya mikusanyiko iliyofuata, moja ilikuwa mahsusi kuhusu uendelezaji wa ustaarabu.
Aya zifuatazo zimenukuliwa kutoka kwenye nyenzo zilizosomewa na washiriki wa makongamano kuhusu mada hii.
Jitihada za Wabahá’í na marafiki zao za kujenga jumuiya siyo tu miradi mizuri ya kijamii ya watu walio tayari kutoa. Zinajengwa juu ya imani kwamba binadamu anaishi katika kipindi cha kipekee sana katika historia yake. Katika maendeleo yake, binadamu amepitia hatua zinazofanana na utotoni na ujana na sasa anasimama mwanzoni mwa ukomavu wake. Mchakato miwili isiyotengana, mmoja wa kusambaratika na mwingine wa kuunganika, inasogeza mbele jamii. Mchakato wa kusambaratika unaonekana katika vurugu, vita na ufisadi vinavyoandamana na kuanguka kwa utaratibu uliochoka ambao hauwezi tena kukidhi mahitaji ya ulimwengu unaokomaa. Unasababisha kuchanganyikiwa na mateso makubwa lakini pia huchangia kuondoa vikwazo vya umoja na watu. Mchakato wa kuunganika unahusiana na nguvu za kiroho zilizochiliwa na ujio wa Bahá’u’lláh. Kwa upande mmoja, nguvu hizi zinaushawishi idadi inayoongezeka ya watu kila mahali wafanye kazi kwa ajili ya umoja na maendeleo. Kwa upande mwingine, zinaunda upya jamii kidogo kidogo kupitia juhudi za makusudi za Wabahá’í na marafiki zao.
...Lengo la kujenga ustaarabu mpya linahitaji mabadiliko kamili katika jinsi jamii inavyojipanga na pia katika mienendo na tabia ya watu binafsi. Katika uhusiano huu, mafundisho ya Bahá’u’lláh yanakusudia “kuleta mabadiliko katika tabia nzima ya mwanadamu, badiliko ambalo litajidhihirisha wazi, la nje na ndani, litakalogusa maisha ya ndani na hali za nje.”
Cha lazima katika ujenzi wa ustaarabu ni kukubali kwamba watu wote wa dunia, kwa kweli wa kila jamii, ni kitu kimoja. Kutambua ukweli huu wa muhimu kuna athari nyingi kwenye maisha ya jumuiya na jamii pana. Katika siku hii, watu wote wa dunia wamepokea kipimo sawa cha fadhila na rehema za Mungu wa kweli na, katika utofauti wao, wanashiriki haki na jukumu la kuchangia kujenga dunia mpya. Mawasiliano kati ya washiriki wa jumuiya, na pia kati yao na taasisi, yakiwa yamejaa upendo na haki, wote hupata fursa ya kutumia sifa walizopewa na Mungu kukuza maendeleo ya kijamii. Maarifa ya kiroho na ya kisayansi yanapopatikana kwa wote, wanajumuiya wanaweza kujifunza pamoja jinsi ya kuyatumia katika maisha yao ya pamoja. Hili linaendana na jitihada za ujenzi wa jamii za Wabahá’í zilizoelezwa katika tamko lililopita ambazo zinaongezeka katika makundi mengi, mitaa, na vijiji duniani kote. Mabadiliko ya utamaduni wanayochochea ni ushahidi wa jinsi jamii mpya inavyochipuka kutokana na jitihada za watu wengi kutumia mafundisho ya Mungu wa siku hii katika maisha ya jumuiya nyingi zinazokua.
Athari zake kwa maisha ya mtu binafsi anayetamani kuchangia katika kuendeleza ustaarabu pia ni kubwa. Mtu hulenga kupata sifa, mielekeo na uwezo wa kuwa mchangiaji bora wa maendeleo na kuwambatanisha vipengele mbalimbali vya maisha yake—elimu, kazi, ndoa, maisha ya familia—kupitia hisia kali ya dhamira. Mtu kama huyo hufanya kila jitihada kulingana na viwango vya Imani. Kujifunza kuepuka chuki za aina zote, kushikamana na kiwango cha juu cha usafi wa mwenendo, na kuonesha unyoofu katika mahusiano na wengine humwezesha mtu kuwa mchezaji bora wa jitihada za kubadili jamii. Katika “jitihada za kujikuza binafsi na kushikilia viwango vya Kibahá’í,” yeye hupata kujihusisha na jumuiya inayolenga madhumuni, mazingira ambapo umoja wa kweli huwasukuma marafiki wa rika zote kusaidiana kufikia viwango vya juu zaidi vya ubora kiroho, kimaadili, na kiakili.
Kutoka mtazamo huu, basi, anayefahamu uwezo wa kuubadili ulimwengu upya uliobebwa na ujumbe wa Bahá’u’lláh bila shaka atapata furaha kubwa kuleta msukumo wa ujumbe huo kwa watu wa dunia, na kuwawezesha kuinuka kutimiza wajibu wao kama wajenzi wa makusudi wa ustaarabu mpya.
Maswali ya tafakari
Vijana chini ya hali anuwai za kijamii wanawezaje kuhakikisha wanapata elimu bora zaidi inayowezekana? Je, kazi au taaluma ya mtu binafsi itawezaje kutumika kama njia ya kuchangia ujenzi wa ustaarabu? Ni nini kingefanya iwe kizingiti?
Vijana wanawezaje kujiandaa vyema kwa ajili ya ndoa na familia zitakazochangia kikamilifu kujenga jamii mpya?
Jumuiya ya mahali pa aina gani ingeweza kusaidia wanajamii wake kukuza sifa na uwezo wa kujenga ustaarabu?
Vijana, ambao mzigo wa kazi ya kujenga dunia mpya unategemea wao zaidi, wanawezaje kujisaidia kwa ufanisi ili kufanikisha maendeleo katika maeneo yote ya maisha yao?









