Imani Ya Kibahá’í

Tovuti ya jumuiya ya Kibahá’í ya kiulimwengu

Kile Wabahá’í wanachofanya

Vijana

Nyenzo kutoka kwenye makongamano ya vijana

Ujana wa awali

Kundi la vijana saba wakiimba pamoja

Miongoni mwa mada zilizochunguzwa wakati wa mfululizo wa makongamano ya vijana duniani kote mwaka 2013 na mawimbi ya mikusanyiko iliyofuata, moja ilikuwa mahsusi ikihusiana na nguvu na uwezo vinavyochomoza katika kipindi cha ujana wa mapema.

Aya zifuatazo zimenukuliwa kutoka kwenye nyenzo zilizosomewa na washiriki wa makongamano kuhusu mada hii.

Wakiangukia kati ya umri wa miaka 12 hadi 15 na wakiiwakilisha hatua ya mpito kutoka utoto kwenda ujana, vijana wadogo—wanaoitwa “vijana chipukizi”—hupitia mabadiliko ya haraka ya kimwili, kiakili, na kihisia. Nguvu zao za kiroho huongezeka. Kiwango kipya cha utambuzi huchochea ndani yao hamu ya kuuliza maswali mazito na kukuza vipaji na uwezo wao. Wakati huu mfupi na muhimu wa miaka mitatu, mawazo kuhusu mtu binafsi na jamii ambayo yanaweza kuitengeneza sehemu kubwa ya maisha yao huundwa. Hata hivyo, furaha ya nguvu hizi mpya huenda ikaambatana na wasiwasi, kutokujisikia vizuri, na shaka ambavyo vinaweza kuleta tabia za kupingana. Kuielekeza nguvu hii mpya kwenye huduma isiyo na ubinafsi kwa wanadamu ni hitaji la muhimu kwa umri huu.

Mitazamo fulani juu ya vijana chipukizi haioni hatua hii ya maisha katika mwanga chanya. Mitazamo maarufu, kwa mfano, huiangalia hatua hii kama iliyojaa kuchanganyikiwa na misukosuko. Mawazo kama haya hueneza mazingira yatakayofanya tabia zisizopendeza kusambaa. Uelewa sahihi wa umri huu ni ule wa vijana wasio na ubinafsi wenye “hisia kali za uadilifu, hamu ya kujifunza kuhusu ulimwengu na shauku ya kuchangia ujenzi wa dunia bora zaidi”. Sifa mbaya wanazozionesha mara nyingine si za kiasili kwa hatua hii ya maisha ya mwanadamu.

Jambo muhimu la kuzingatia basi ni chanzo cha tabia zisizokubalika ambazo mara nyingine huonekana kwa vijana chipukizi. Kuna mambo mawili ya kuzingatia sana hapa. Kwanza, athari za nguvu hasi za kijamii kwenye jamii nyingi zimesababisha kuenea kwa matatizo ya kijamii yenye ushawishi mkubwa juu ya namna vijana wanavyojiona na kuona jamii. Pili, vijana chipukizi huathiriwa mno na tabia ya watu wazima kuelekea kwao. Ingawa katika umri huu wanapata uelewa wa mambo mengi mazito, watu wazima wakati mwingine husisitiza kuwachukulia kama watoto. Aidha, tofauti kati ya maneno na matendo inayooneshwa mara kwa mara na watu wazima baadhi inaweza kuwa chanzo cha kuchanganyikiwa kwa vijana wanaotafuta viwango vya kujipimia maisha.

Kusisitiza athari za nguvu hasi kwa vijana chipukizi haimaanishi kwamba vijana ni dhaifu asili yao. Wanaweza, kwa msaada, kuelea nguvu hizo. Wanaweza kukuza nguvu za roho na akili ambazo zitawapa uwezo wa kuyashinda na pia kuwafanya wachangie kwenye ujenzi wa jamii mpya.

Maswali ya tafakari

Katika kutafakari juu ya vijana chipukizi katika jumuiya yako, zungumza jinsi wanavyoathiriwa na nguvu mbovu na tabia zinazochipuka kutokana nayo.

Elezea jinsi vijana chipukizi katika jumuiya yako wanavyoendelea kiroho na kiakili na jinsi wanavyojifunza kuchangia maendeleo ya familia na jumuiya zao.

Zungumzia sifa za kiroho na mielekeo unayodhani mtu anayewasaidia vijana chipukizi anapaswa kujitahidi kuonesha.

Chunguza nyenzo kutoka kwenye makongamano ya vijana

Unaweza kusoma zaidi kuhusu mada hii katika makala zifuatazo.