Kile Wabahá’í wanachofanya
Vijana
Nyenzo kutoka kwenye makongamano ya vijana
Ujenzi wa Jamii na Kukuza Msaada wa Mmoja kwa Mwingine
Miongoni mwa mada zilizochunguzwa wakati wa mfululizo wa makongamano ya vijana yaliyofanyika duniani kote mwaka 2013 na mawimbi ya mikusanyiko iliyofuata, ziliibuka pia mada zinazohusu ujenzi wa jumuiya na kukuza kusaidiana.
Aya zifuatazo zimenukuliwa kutoka kwenye nyenzo zilizosomewa na washiriki wa makongamano kuhusu mada hizi.
Jukumu kubwa la kuchangia kwenye ustawi wa jamii linakabili kizazi cha sasa cha vijana. Pia kwao kunategemea jukumu la kukuza mazingira ambayo washiriki wachanga wa jamii wanaweza kufikia nguvu za kiroho na kiakili za kuwa wajenzi wa ustaarabu mpya. Jukumu hili ni kubwa bila shaka. Ili kupambana na nguvu kali za kijamii zinazotishia kumomonyoa nguvu zao na kupotosha malengo yao, vijana wanaweza kutegemea msaada wa Mungu usiokoma. Wanapaswa pia kuongeza uwezo wa kuunda mazingira ya kusaidiana na kusaidiana wao kwa wao na jumuiya zao ambapo nguvu zao za kubadilisha jamii huzidishwa.
Sasa unatakiwa kutafakari juu ya mchango ambao kizazi chako kinaweza kufanya katika kujenga jumuiya hai katika mitaa na vijiji, na pia maeneo mengine ambapo watu wenye hamu ya kujihusisha na mabadiliko ya pamoja wanapatikana.
Ili kuzingatia swali hili, ni muhimu kupitia kwa kifupi baadhi ya vipengele vya mfumo wa utekelezaji unaoongoza juhudi za jumuiya ya Kibahá’í duniani kote. Shughuli nyingi za jumuiya za Wabahá’í za kujenga jamii mpya inayotokana na mafundisho ya Bahá’u’lláh hufanyika katika muktadha wa kundi, eneo dogo linaloweza kudhibitiwa kijiografia linalojumuisha vijiji na pengine mji mdogo au jiji kubwa na vitongoji vyake. Lengo kuu katika kila kundi ni kuimarisha, kupitia matumizi ya mafundisho ya Kibahá’í, wahusika watatu wakuu katika mchakato wa mabadiliko: mtu binafsi, jumuiya, na taasisi. Kazi hii inahusisha kulea, kupitia mchakato wa taasisi, idadi inayoongezeka ya watu wenye uwezo wa kukuza maendeleo ya kiroho na kijamii; kujenga jumuiya hai za mahali ambapo “watu binafsi, familia na taasisi … [wanashirikiana] kwa lengo moja kwa ajili ya ustawi wa watu ndani na nje ya mipaka yake”; na kukuza taasisi zilizo na uwezo wa kuwezesha, kuelekeza na kuunganisha nguvu za marafiki wengi wanaotamani kuhudumu. Makundi haya huweza kuwa kwenye hatua tofauti za maendeleo kulingana na idadi na ufanisi wa wale wanaofanya kazi ya mabadiliko na nguvu na maendeleo ya jumuiya na taasisi zake za mahali. Katika baadhi yake, juhudi za Wabahá’í za kujenga jamii mpya bado hazijaanza.
Kila kundi, marafiki wanakutana na mazingira tofauti. Wengi wao wanaishi katika vijiji vingi vilivyo na ufanano mkubwa, au kwenye mitaa mbalimbali ya miji mikubwa. Roho ya pamoja huonekana sehemu nyingine; kwingineko, haipo wazi. Marafiki katika kundi wanaweza pia kushirikiana na wengine kutokana na maslahi fulani ya pamoja, kwa mfano, kusoma katika chuo kikuu au uanachama kwenye shirika la kitaaluma au kijamii lisilohitaji uwepo wa mahali pamoja. Ili kujenga jamii mpya, marafiki hutafuta kukuza uwezo wa kutumia mafundisho ya Bahá’u’lláh katika mazingira na sehemu hizi. Hakuna jamii inayoweza kupata maendeleo ya kiroho na kijamii yanayowezekana katika enzi hii ya uhai wa binadamu bila huduma isiyo na ubinafsi ya wanajumuiya wake.
Katika kutafakari juu ya jitihada za kizazi kipya kutembea njia ya huduma, ni muhimu kufikiria namna gani wanaweza “kukuza maisha hai ya kijumuiya katika mitaa na vijiji”.
Maswali ya tafakari
Unaonaje asili halisi ya urafiki? Ungejuaje ni urafiki upi unasaidia na upi hausaidii maendeleo ya vijana?
Kujenga mazingira ya kusaidiana kunajumuisha kuwa na maono ya idadi kubwa ya vijana ambao, kama marafiki wa kweli, wanashirikiana kubadili jumuiya yao. Utafanyaje kutekeleza maono kama hayo katika kundi au jumuiya yako? Mazungumzo miongoni mwa vijana yatakuwa ya muhimu kiasi gani, na nini lengo na maudhui yake?
Mchakato wa ujenzi wa jamii unaoongozwa na ujumbe wa Bahá’u’lláh lazima ue na msingi wa mazungumzo yanayoendelea kuhusu mafundisho ya Imani na athari zake katika maisha ya watu. Unaweza kufanya nini kuhamasisha idadi kubwa ya vijana kuwa sehemu ya mazungumzo haya na mchakato muhimu wa kujifunza na huduma unaohusiana nayo?
Vijana wana mchango gani wanaoufanya, au wanaweza kuuongeza, ili kuimarisha michakato ya mashauriano ndani ya jumuiya yako?







